Wakazi wa Mumias Mashariki waandamana juu ya NG-CDF

Martin Mwanje
1 Min Read

Baadhi ya wakazi wa eneo bunge la Mumias Mashariki wameandamana kulalamikia uamuzi wa Mahakama Kuu kusitisha utekelezaji wa Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) ifikapo mwaka 2026.

Wakazi hao wanadai kuwa uamuzi wa mahakama unakiuka katiba.

Wamesisitiza kuwa wamepata manufaa mengi kupitia hazina hiyo, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu na kusaidia kugharimia masomo ya wanafunzi kutoka familia maskini.

Aidha, wametoa wito kwa wabunge kuhakikisha uamuzi wa mahakama unabatilishwa na hazina hiyo kuendelea kuwepo.

Wanadai wengi wao wanapata msaada wa haraka kutoka kwa wabunge ikilinganishwa na huduma za serikali za kaunti.

Mahakama Kuu wiki iliyopita ilitangaza NG-CDF iliyobuniwa mwaka 2015 kuwa kinyume cha katiba.

Ikiharamisha hazina hiyo, mahakama hiyo iliagiza kuwa huduma za hazina hiyo pamoja na miradi yake inayoendelea zitasitishwa Juni 30, 2026.

Share This Article