Wahudumu wa afya wahimizwa kujifunza lugha ya ishara

Boniface Musotsi
2 Min Read

Shirika la kutetea haki za walemavu haswa la This Ability Trust, limetoa wito wa somo la lugha ya ishara kujumuishwa katika somo la matibabu, ili kurahisisha mawasiliano baina ya wahudumu wa afya na wagonjwa wenye walemavu.

Kwa mujibu wa shirika hilo ambalo limekuwa litoa mafunzo ya ishara kwa wanawake wanaoishi na ulemavu katika kaunti ndogo ya changamwe, lilitaja kuwa wazazi hupata changamoto nyingi wanapowapeleka wanao wenye ulemavu kwani wahudumu hao hawafahamu lugha ya ishara.

Aidha, afisa mkuu wa shirika hilo Florence kaha, alidokeza kuwa, ‘’wanawake wenye ulemavu haswa wajawazito, wanakumbana na changamoto wanapotafuta huduma za afya kwani hawahudumiwi kama wengine. Wengi wanahdumiwa kwa dharau, kushambuliwa, kupelekwa kwenye chumba cha upasuaji ilihali wanaweza kujifungua vyema’’.

Aliongeza kuwa, ‘’ Tunataka hospitali zote ziwe na wakalimani wa lugha za ishara na ikiwezekana somo hilo lijumuishwe kwenye mfumo wa somo la afya ili wahudumu hao wawasiliane na watu wanaoishi na ulemavu – PLWDs. Unaweza pata kiziwi amepewa dawa isiyo stahili kwa sababu hawaelewi lugha’’.

Pia alifichua kuwa baadhi ya hospitali huwalazimisha wagonjwa wa kike kutumia njia za kupanga uzazi wasizopenda.

Ni kwa msingi huu ndiposa shirika hilo liliazimia kutoa mafunzo ya ishara kwa wadumu wa afya 185 katika vituo vya afya 22 ya jinsi ya kushughulikia walemavu hao. Vile vile, limebuni kikundi cha mawakili kungamua mahitaji muhimu.

Shirika hilo lilitoa nambari ya simu kwa jina Mama siri (0800 000 300) ili walemavu hao waripoti visa mbalimbali bila malipo na kupata huduma ya dharura kutoka hospitalini.

Boniface Musotsi
Share This Article