Wakazi wengi wa eneo la Fort Nelson, British Columbia nchini Canada wameagizwa kuondoka kwenye makazi yao kutokana na tishio la moto mkubwa.
Moto huo unaripotiwa kuzuka Ijumaa usiku na maafisa waliutaja kuwa hatari kiasi kwamba tahadhari imetolewa hata katika mkoa jirani wa Alberta.
Serikali ya Canada imeonya kwamba hali ya anga mwaka huu huenda ikasababisha ongezeko la hatari ya moto nchini humo.
Moto huo katika eneo la Ziwa Parker ulitangazwa na idara inayosimamia dharura za moto katika eneo la British Columbia na kufikia Jumamosi asubuhi ulikuwa umesambaa kwa kasi na kuathiri eneo la kilomita nane mraba.
Watu wapatao elfu 3 wameagizwa kuhama eneo hilo.
Meya wa eneo la Nothern Rookies Rob Fraser, aliambia wanahabari kwamba moto huo ulianza baada ya upepo mkali kung’oa mti ambao uliangukia nyaya za stima na kushika moto.
Aliongeza kwamba wazima moto walipofika walipata umesambaa sana wakashindwa kuudhibiti kwa kutumia vifaa walivyokuwa navyo kwani upepo mkali na hali ya ukavu ninachangia moto huo kusambaa kwa kasi.
Helikopta tisa zilihusishwa katika juhudi za kuzima moto huo huku wafanyakazi wengi pia wakijibidiisha kuudhibiti ardhini.
Mwaka jana Canada ilifikwa na visa vingi vya moto kwenye misitu ambapo hekta milioni 15 za misitu ziliharibiwa kabisa. Wazima moto wanane waliaga dunia kwenye visa hivyo vya mwaka jana huku wengine 230,000 wakipoteza makazi.