Wakazi Mandera wahimizwa kupanda miti kwa wingi

2 Min Read

Kamishna wa kaunti ya Mandera Amos Mariba amehimiza wakazi wa kaunti hiyo kupanda miche ya miti kwa wingi sio tu leo bali siku zote.

Akizungumza alipoongoza shughuli ya upanzi wa miche ya miti katika taasisi ya mafunzo ya kimatibabu KMTC, Mariba alisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuanzisha eneo la kukuza miche ya miti akisema hatua hiyo itapunguza gharama ya kununua miche hiyo.

Mariba aliongoza shughuli hiyo iliyofanyika katika maeneo yote nchini kama hatua ya kutafuta kuafikia lengo la Rais William Ruto la upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Kulingana na kamishna huyo, muche elfu 45 ilipandwa leo huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kufikia mwisho wa siku hii iliyotengwa na serikali kwa upanzi wa miti.

Naibu Gavana wa kaunti ya Mandera Ali Maalim alishukuru serikali ya kitaifa kwa kuongoza shughuli hiyo akisema inaweza kuboresha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo.

Aliahidi usaidizi wa serikali ya kaunti katika utekelezaji wa shughuli hiyo na akapendekeza iendelezwe hadi kwenye kaunti ndogo.

Kaunti ya Mandera inalenga kupanda miche milioni 160 kulingana na maelekezo ya serikali ya kitaifa.

Kiwango cha misitu katika kaunti hiyo kwa sasa ni asilimia 2.06 huku kiwango cha misitu nchini kikiwa asilimia 7.

Serikali imetenga milioni 80 mwaka huu wa matumizi ya pesa za serikali kuimarisha mipango ya kuongeza kiwango cha misitu.

Website |  + posts
Share This Article