Wakazi Bungoma wahimizwa kususia siasa za upinzani

Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula anawataka waunge mkono azma ya Rais Ruto ya uchaguliwa kwa muhula mwingine.

Marion Bosire
1 Min Read

Spika wa bunge la taifa Moses Masika Wetangula, amehimiza wakazi wa kaunti ya Bungoma, hususan vijana wasusie siasa za upinzani.

Badala yake Wetangula anawataka waunge mkono azma ya Rais William Ruto kuchaguliwa tena mwaka 2027 na kujiepusha na siasa za upinzani anazozitaja kuwa zisizo na tija.

Wetangula alitoa matamshi hayo alipoungana na familia, marafiki na wakazi wa West Nalondo kuomboleza kifo cha Mzee Joseph Wanyonyi Yaola, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 93.

Katika ujumbe wake, Spika huyo aliwataka wakazi kupima uongozi kwa kuzingatia maendeleo yanayoonekana na fursa zinazotengenezwa kwa manufaa ya jamii.

Alitaja ajenda ya maendeleo ya Rais Ruto katika Kaunti ya Bungoma, kama vile kuboreshwa kwa miundombinu, huduma muhimu, uwezeshaji wa vijana na ukuaji wa uchumi.

Wetangula pia alihimiza wakazi kuimarisha mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya sasa na kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Ruto mwaka 2027.

Aidha, alifichua wazi azma yake ya kuwania urais mwaka 2032, akisema analenga kujitolea kuongoza nchi wakati huo.

Alisema eneo la Magharibi mwa Kenya linapaswa kujenga ushirikiano wa kimkakati na kuimarisha uhusiano wa kisiasa ili kuongeza nafasi ya eneo hilo katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2032.

Alisisitiza kuwa siasa zinapaswa kuongozwa na maendeleo na mustakabali wa wananchi.

Share This Article