Murkomen: Serikali haitalegeza kamba kwenye vita dhidi ya majangili

Murkomen alisema operesheni hiyo haitakuwa ya muda mfupi kama zile za awali, lakini itakuwa yakudumu katika eneo hilo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Serikali yaahidi kukabiliana na majangili Kerio Valley.

Serikali  imerejelea wito wake kwamba haitalegeza kamba kwenye operesheni ya asasi mbalimbali inayoendelea katika Bonde la Kerio, hadi bunduki zote haramu zitakapotwaliwa na ujangili kutokomezwa.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, alisema operesheni ya Maliza Uhalifu itaendelea hadi mitandao yote ya wahalifu iangamizwe, na wakazi waendeshe shughuli zao bila uwoga.

“Operesheni inayoendelea katika Bonde la Kerio, itaendelea hadi bunduki zote haramu zitwaliwe kutoka kwa majangili,” alisema Murkomen.

Alitangaza kuwa operesheni hiyo haitakuwa ya muda mfupi kama zile za awali, lakini itakuwa yakudumu katika eneo hilo.

“Awali makundi ya usalama yamekuwa yakitekeleza operesheni na kuondoka. Wakati huu, makundi ya usalama yataishi hapa na wakazi. Kufikia mwezi Disemba, operesheni hii itaongezwa mara tatu, huku timu tatu zikitekeleza operesheni Samburu, Kerio ya Kati na Turkana,” aliongeza waziri huyo.

Murkomen alitoa wito kwa wakazi kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kutoa habari zitakazofanikisha kupatikana kwa silaha haramu na kuangamizwa kwa mitandao ya wahalifu.

“Tunatoa wito kwa kila mkazi wa Kerio Valley kushirikiana na maafisa wa usalama kuhakikisha bunduki zote haramu zinatwaliwa ili tuangamize uhalifu,” aliongeza Murkomen.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi  Soipan Tuya, alidokeza kuwa maendeleo ambayo yanashuhudiwa Kerio Valley, yanaashiria ufanisi wa operesheni ya Maliza Uhalifu, mpango wa kiusalama unaojumuisha Vikosi vya Ulinzi (KDF), Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), Idara ya Ujasusi (NIS), Idara ya Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) na Maafisa wa Serikali ya Taifa (NGAO).

Wawili hao walikuwa wakizungumza walipolkuwa wakikadiria hali ya usalama katika Bonde la Kerio pamoja na kuzindua kaunti ndogo ya Kolowa.

Share This Article