Waiguru anatosha wadhifa wa Naibu Rais, wasema wanawake Kirinyaga

Tom Mathinji
1 Min Read
Wanawake kaunti ya Kirinyaga wamuidhinisha Waiguru kwa wadhifa wa Naibu Rais.

Mamia ya wanawake kaunti ya Kirinyaga,  wametoa wito kwa Rais William Ruto kumteua Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru kuwa naibu Rais wa taifa hili.

Wanawake hao walimuidhinisha Waiguru, wakisema ndiye chaguo bora kwa wadhifa huo wa Naibu Rais, iwapo Rigathi Gachagua atabanduliwa katika wadhifa huo.

Wakizungumza mjini Kutus, wanawake hao waliojumuisha viongozi wa kijamii kutoka wadi ishirini za kaunti hiyo, walidokeza kuwa Kenya sasa iko tayari kwa Naibu Rais mwanamke, na Gavana Waiguru anafaa zaidi kwa wadhifa huo.

Walitoa wito kwa kiongozi wa taifa kurejesha wadhifa wa Naibu Rais katika eneo la mlima Kenya, na kumpa mwanamke wadhifa huo ili atimize ahadi yake ya kuwa na naibu mwanamke siku za usoni.

“Kama wakazi wa eneo la mlima na Kirinyaga, tulimuunga mkono kikamilifu Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, na tumhimiza kuwa ikiwa nafasi ya Naibu Rais itapatikana, amteue Gavana Waiguru,” alisema mmoja wa wanawake hao Mary Nyawira.

Nyawira alisema Waiguru ameleta maendeleo mengi katika kaunti ya Kirinyaga, hatua iliyoinua jamii nyingi katika eneo hilo.

“Iwapo fursa hiyo itapatikana tuna uhakika Gavana Waiguru anatajiriba ya kutosha kwa wadhifa huo.” aliongeza Nyawira.

Share This Article