Wahudumu wa matatu wamehimizwa kujiepusha na utumizi wa pombe na mihadarati, kwani zinasababisha changamoto nyingi katika familia changa.
Mke wa Naibu Rais Dorcas Rigathi amesema sekta ya matatu haipaswi kupuuzwa kwa kuwa inatekeleza wajibu muhimu katika jamii.
Dorcas aliyasema hayo katika kaunti ya Kisii, alipozindua kambi ya siku mbili ya matibabu inayowalenga wahudumu wa matatu na wale walioathiriwa na utumizi wa mihadarati katika juhudi zake za kumuinua mtoto wa kiume.
Kambi hiyo ya matibabu pia inalenga familia zinazoishi mitaani katika kaunti ya Kisii.
“Madereva na utingo wa matatu na wengine katika sekta ya matatu, wanapaswa kuheshimiwa kama sehemu ya wanaochochea ukuaji wa uchumi. Wengi wetu tunawathamini na maisha yetu, lakini hatuheshimu kazi yao. Nitatembea nanyi,” alisema Dorcas.
Gavana wa Kisii Simba Arati kwa upande wake alipongeza juhudi za mkewe Naibu Rais za kumuinua mtoto wa kiume akisema hatua hiyo inasaidia pakubwa kuokoa kizazi kilichoko.
Dorcas Rigathi yuko katika kaunti ya Kisii kwa ziara rasmi ya siku tatu.