Wafanyabiashara Garissa waonywa dhidi ya kuhodhi bidhaa za chakula

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Garissa Nathif Jamah ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaotumia mafuriko yanayoshuhudiwa katika kaunti hiyo kwa sasa kuhodhi bidhaa muhimu akisema leseni zao zitafutiliwa mbali. 

Nathif alisema ofisi yake imepokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wakazi wanaolalamika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanahodhi bidhaa muhimu na kusababisha uhaba wa bidhaa hizo.

Kisha baadaye, wanapandisha bei ya bidhaa hizo na kujipatia faida kubwa kwa sababu barabara kuu za kupeleka chakula katika kaunti hizo zimefungwa.

Katika kipindi cha siku tatu zilizopita, mamlaka ya kitaifa inayosimamia barabara kuu nchini, KeNHA imefunga kwa muda barabara kuu za Garissa – Nairobi na Garissa – Mombasa baada ya sehemu za barabara hizo kusombwa na mafuriko.

Akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja mjini Garissa, Nathif alisema baadhi ya bidhaa zinazohodhiwa ni pamoja na sukari, maziwa, unga wa mahindi na mafuta ya kupikia miongoni mwa  zingine.

Alitaja kuhodhiwa kwa chakula kuwa kitendo cha uhalifu akiahidi kuwachukulia wahusika hatua kali.

Share This Article