Wafanyabiashara mjini Naivasha walalamikia biashara duni licha ya Safari Rally

Dismas Otuke
1 Min Read

Wafanyabiashara mjini Naivasha wamelalamikia biashara zao kuwa chini kinyume cha matarajio ya kwamba vingenoga kutokana na mashindano yanayoendelea ya magari ya Safari Rally.

Baadhi ya wale tuliosema nao hasa wa vyumba vya kupangisha waliongeza bei kwa kati ya shilingi 500 na 2000 wakitarajia ongezeko la wateja.

Hata hivyo, licha ya mashindano kuandaliwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka kwa mara ya kwanza baada ya subira ya miaka 26, watu wengi hawakufurika kuyafuatilia.

Baadhi ya mashabiki walihiari pia kutundika hema karibu na vituo ambavyo magari yanashindana masafa marefu kutoka mjini.

Pia hatua ya serikali kupiga marufuku uuzaji vileo katika maeneo ya mashabiki kusimama ili kufuatilia mashindano, kumeathiri pakubwa wauzaji tembo.

Badala yake, mashabiki wengi wa Safari Rally wanahiari kununua vileo vyao kutoka mjini Naivasha.

Kwa kifupi, athari ya mashindano hayo yanayoandaliwa Naivasha kwa mara ya nne mtawalia, haijakuwa kubwa kwa wajasiriamali.

Mashindano hayo yameingia siku ya pili leo Ijumaa huku madereva wakishindana katika vituo vitatu vya Loldia, Geothermal na Kedong.

Share This Article