Wachukulieni hatua polisi wafisadi, aagiza Koskei

Martin Mwanje
1 Min Read
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei

Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome ameagizwa kufanya kila awezalo kuhakikisha maafisa wanaowapora Wakenya pesa zao wakati wa zoezi la kuwaajiri maafisa wapya wa polisi wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali.

Koskei amelalama kuwa zoezi la kuwaajiri maafisa wapya wa polisi limegeuka kuwa biashara ambapo baadhi ya maafisa huitisha hongo ya hadi shilingi elfu 60 kutoka kwa wanaotaka kujiunga na huduma ya polisi.

“Serikali inafahamu kuwa zoezi la kuwaajiri maafisa wapya wa polisi limegeuka kuwa biashara ambapo wanaotaka kusajiliwa hutakiwa kulipa kitita kikubwa cha fedha ili kujiunga na huduma ya polisi,” alilalama Koskei.

“Inspekta Mkuu wa Polisi anapaswa kuingilia kati na kuwachukulia hatua kali maafisa wachache wa polisi wanaowapora Wakenya fedha zao walizozipata baada ya kutokwa na kijasho chembamba.”

Wakati huohuo, Koskei amewataka maafisa wa ngazi ya juu katika idara ya polisi kutokomeza ufisadi katika vizuizi vikuu barabarani.

“Wakati umewadia kwa maafisa wa polisi waliopo barabarani kuanza kutekeleza majukumu yao badala ya baadhi ya maafisa kutumia mamlaka yao kutafuta rushwa.”

Koskei aliyasema hayo wakati wa mkutano wa ushauriano na maafisa wa Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS leo Ijumaa.

 

Share This Article