Wabunge wazuru Kilgoris na Kuria Mashariki kujionea hali ya usalama

Marion Bosire
2 Min Read
Gabriel Tongoyo, mwenyekiti wa kamati ya utawala na usalama wa taifa bungeni

Wanachama wa kamati ya bunge la taifa kuhusu utawala na usalama wa ndani ilizuru maeneo ya Angata Barikoi na Nyaderema huko Kilgoris na Kuria Mashariki kujifahamisha kuhusu hali ya usalama.

Wakiongozwa na mwenyekiti Gabriel Tongoyo mbunge wa Narok Magharibi, wabunge hao walitagusana na wananchi katika vikao wakitafuta kufahamu kinachosababisha migogoro na njia za kusuluhisha.

Kamati hiyo ilitoa gari jipya la polisi kwa kundi la usalama la Angata Barikoi kama njia ya kutambua kujitolea kwa kundi hilo kuhakikisha amani huku kukiwa na changamoto mbali mbali.

Naibu kamishna wa eneo hilo Muhammed Jubat, alizungumza juu ya migogoro ya mara kwa mara kati ya jamii za Kuria na Kipsigis kuhusu ardhi ya ukubwa wa ekari 6,300.

Wakazi walisimulia kuhusu matokeo ya migogoro hiyo kama vile vifo 17, majeruhi kadhaa na mzigo wa kifedha kwa familia kutokana na bili za hospitali.

Wanapata hasara pia kufuatia kuharibiwa kwa mimea shambani pamoja na mauaji ya mifugo.

Ben Koiyando, kiongozi wa chama cha ushirika cha wakulima cha Angata Barikoi alitoa maelezo ya kihistoria akisema kwamba ardhi hiyo ilikuwa ya jamii ya Maasai kabla ya kuuziwa jamii mbali mbali.

Wakazi wa Gwitembe walionyesha wasiwasi kuhusu mvutano huo wakisema awali waliishi vizuri na wenzao wa jamii ya Kipsigis lakini sasa wanahisi jamii yao ya Kuria imetelekezwa.

Watu wa Gwitembe walipendekeza kutengwa kwa eneo huria kati ya maeneo ya Gwitereri na Gututa na kuondolewa kwa kambi ya GSU katika maeneo yanayozozaniwa.

Walipendekeza pia malipo ya fidia kwa waathiriwa wa ghasia, kukamatwa kwa wachochezi na kuundwa upya kwa mipaka.

Katika soko la Kugitimo wakazi waliomba kurejeshwa kwa ekari 20 za ardhi wanayodai kupokonywa kama njia ya kuzuia migogoro zaidi.

Baada ya kuskiliza wahusika wote, wanachama wa kamati hiyo ya bunge walijitolea kuandika ripoti itakayowasilishwa bungeni huku wakishinikiza kuafikiwa kwa suluhisho ili kurejesha amani na usalama katika eneo hilo.

Website |  + posts
Share This Article