Wabunge walalamikia huduma mbovu za SHA

Martin Mwanje
1 Min Read

Katibu katika Wizara ya Afya Harry Kimutai na mwenyekiti wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) Dkt. Abdi Mohammed walikuwa na wakati mgumu kutetea utekelezaji wa mpango huo unaokumbana na changamoto za kila aina walipofika mbele ya wabunge. 

Wabunge hususan walitemea hisia zao juu ya mpango huo wakati wa mkutano wao unaoendelea mjini Naivasha, wakilalamikia kutopatikana kwa huduma muhimu katika maeneo bunge yao huku ikiwa si bayana SHA inagharimia huduma zipi.

“Kuna watu milioni 18 waliojisajili na wanajua kwamba wamejisajili kwa hivyo wanapaswa kupata huduma lakini hawapati huduma hizo. Wizara inapaswa kuchukua hatua kuhusu hili,” alilalama mbunge wa Seme James Nyikal.

“Wizara inapaswa kuwasiliana kwa usahihi. Tunahitaji kufahamu hasa SHA inagharimia nini?” aliongeza mbunge wa Teso Kusini Mary Emaase.

Kwa upande wake, Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alilalamikia hatua ya kumkamata Grace Njoki, mwanamke aliyevamia ofisi za Wizara ya Afya akilalamikia huduma mbovu za SHA.

“Kwa nini mwanamke mzee alikamatwa kwa kuelezea kuhangaika kwake* Hapaswi kukamatwa?” alilalama mbunge huyo anayefahamika kwa kutetea haki za wanawake na watoto.

Mpango wa SHA umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi tangu kuzinduliwa kwake huku Wakenya wakilalamika kuwa hawapati huduma muhimu wanapoenda hospitalini.

Serikali inasema inashughulikia changamoto ibuka.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *