Waandamanaji watatiza usafiri barabara ya Nairobi Expressway

Martin Mwanje
2 Min Read

Baadhi ya huduma za ulipiaji ada kwenye barabara ya Nairobi Expressway zimesitishwa kwa muda baada waandamanaji wanaoshiriki maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga kuharibu vituo vya ulipiaji wa ada.

Kampuni ya MOJA Expressway ilitangaza kusitishwa kwa huduma katika vituo vya ulipiaji ada vya Mlolongo, Syokimau na SGR.

Katika taarifa, inasema jitihada zinafanywa kurejesha hali ya kawaida.

Picha ya video iliyosambaa mitandaoni inawaonyesha vijana wakivuta kizuizi kwenye barabara hiyo karibu na kituo cha Mlolongo.

“Tunasikitika kuwataarifu kuwa sehemu ya huduma za ulipiaji ada kwenye barabara ya Nairobi Expressway zimesitishwa kwa muda katika vituo vya vya Mlolongo, Syokimau na SGR kutokana na maandamano yanayoendelea,” ilisema kampuni ya MOJA Expressway kwenye taarifa.

Kutokana na hali hiyo, wasafiri wanaotumia barabara ya Westlands kuelekea Mlolongo wameshauriwa kuondoka kwenye barabara hiyo kwa kutumia kituo cha Jomo Kenyatta International Airport (JKIA).

Wale wanaokumbana na kisa chochote au ajali wanashauriwa kupiga simu kwa namba ya uokozi ya moja kwa moja inayohudumu wakati wote ambayo ni  0111 039888 ili kusaidiwa.

Visa vya uvunjaji sheria na uharibifu wa mali pia vimeshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi na kuwalazimu polisi kurusha vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Taarifa zimeashiria kuwa mtu mmoja amefariki katika vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano hayo.

Website |  + posts
Share This Article