Waandalizi wa tamasha la Furaha City lililofanyika Nairobi Disemba 7, 2024 wametoa taarifa kuhusu kilichotokea humo huku wakijutia kukosa kwa Diamond Platnumz kutumbuiza.
Kulingana nao, juhudi zao za kumpa nafasi Platnumz na kundi lake ziliambulia patupu kwani mienendo yao na mahitaji yasiyo na msingi vilisababisha akose kutumbuiza jinsi ilivyokuwa imepangwa.
Waandaaji hao wanatambua na kukubali kwamba kulitokea tatizo la kiusalama lililohusisha msanii mwingine lakini lilisuluhishwa haraka na halikuhujumu tamasha kwa vyovyote.
Taarifa hiyo ilithibitisha kujitolea kwa waandaaji wa matamasha kuwachukulia wasanii wote kwa usawa na kuhakikisha viwango vya hali ya juu muda wote wa tamasha.
Mafanikio ya tamasha hilo yaliyotajwa na waandalizi kwenye taarifa yao ni pamoja na maonyesho ya kipekee kutoka kwa wasanii wa Kenya na wanajivunia hilo.
“Tunaheshimi msimamo wa Diamond Platnumz kama msanii mkubwa, lakini pia tunatarajia utaalamu na heshima katika pande zote mbili kwenye ushirikiano kama huu.” walisema waandalizi wa tamasha hilo.
Huku wakishukuru mashabiki waliohudhuria tamasha hilo, waandalizi hao wanatumai kwamba siku za usoni matatizo kama hayo yatasuluhishwa kwa njia ya amani na watapata mafunzo kutoka kwayo.
Waliwashukuru pia wasanii wengine wa Tanzania waliotumbuiza kwenye hafla hiyo ambao ni Rayvanny na Zuchu.