Wakazi wa eneo lilalozunguka bonde la Nyankara katika kitongoji cha Pamila Kijiji cha Pamila kata ya Matendo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wamejawa na hofu kufuatia kuonekana kwa tope zito wakidhania kwamba ni volkano.
Wakizungumza kwenye kikao cha kamati ya usalama ya eneo husika, viongozi wa kijiji walielezea kwamba hali hiyo ilianza kwa kiwango kidogo cha tope na baadaye likaongezeka wakidhani chanzo ni kidimbwi cha kufugia samaki kilichotengenezwa hapo karibu.
Tope hilo lilitokea katikati ya kidimbwi hicho na kusababisha samaki wote waliokuwemo kufa na hatimaye kidimbwi kizima kikafunikwa na tope ambalo lilienea kwenye sehemu kubwa.
Hata hivyo mtaalamu mmoja wa masuala ya miamba na jiolojia kutoka afisi ya madini katika mkoa wa Kigoma kwa jina David William Ndosi ameelezea kwamba hiyo ni volcano ya mchanga na maji ambayo kitaalamu inajulikana kama “sand volcano eruption” na haina moto kama volkano nyingine.
Ndosi aliwataka wakazi wa eneo hilo kuondoa wasiwasi akisema nyingi ya volkano kama hizo huatokea kwenye maeneo yenye bonde la ufa na mitetemeko kutokana na kutikiswa kwa miamba.
Hali hiyo husambabisha mchanga na chembechembe za maji zinazotengeneza tope kupanda juu lakini akafafanua kwamba tope hilo halina madhara ila linaweza kuzamisha watu na wakapoteza maisha.
Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amewataka wakazi wa Kijiji cha Pamila kutahadhari na kuacha kusababisha taharuki kupitia taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo.