Chama cha watumiaji wa mahakama ya Malindi inayoshughulika na maswala ya watoto, kimeelezea wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya dhuluma dhidi ya watoto katika kaunti ndogo za Malindi na Magarini kaunti ya Kilifi.
Chama hicho kikiongozwa na hakimu mkuu wa Malindi Elizabeth Usui, kilisikitika kuwa idadi ya visa vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto huenda vikaongezeka wakati huu wa likizo, huku kikitaka wazazi wawe waangalifu kuhakikisha watoto wao wanalindwa.
Siku ya Ijumaa wanachama wa chama hicho pamoja na wadau wengine waliandaa hafla ya kutoa hamasisho kuhusu haki za watoto mjini Malindi na vituo kadhaa vya kibiashara vya Magarini.
Kulingana na hakimu huyo mkuu, visa 139 vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto vilinakiliwa katika makahama ya Malindi tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Alisema idadi hiyo ni ongezeko ikilinganishwa na visa 96 vilivyonakiliwa katika mahakama hiyo.
“Mwaka uliopita tulishughulikia kesi 96 za dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto, lakini mwaka huu kesi hizo zimeongezeka hadi 139 ilhali mwaka haujakamilika,” alidokeza hakimu huyo mkazi.
Alisema watoto wa jinsia zote mbili wamedhulumiwa, lakini akadokeza kuwa watoto wa kike wamedhulumiwa zaidi baada ya kushawishiwa na wanaume au jamaa wa karibu.
“Kesi nyingi ambazo huwa tunashughulikia zinawahusu watoto wasichana, lakini pia visa kuhusu watoto wa kiume vinaongezeka,” alidokeza Usur.
Afisa wa maswala ya watoto kaunti ndogo ya Malindi Sebastian Muteti, kwa upande wake alihusisha dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto na utovu wa maadili katika jamii.
Aidha Muteti alidokeza kuwa visa vingi ya dhuluma dhidi ya watoto huwa haviripotiwi, huku akitoa wito kwa wadau kutumia vilivyo mwezi huu wa huduma kwa watoto kuhusisha jamii katika swala hilo.