Viongozi wa serikali jumuishi kutoka Nairobi leo Ijumaa wamekutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Waliokutana na Rais Ruto ni viongozi kutoka chama tawala cha UDA na kile cha ODM.
Gavana wa kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga na kiongozi wa walio chache katika Bunge la Taifa Junet Mohamed ni miongoni mwa waliohudhuria.
Wengine ni wabunge Phelix Odiwuor wa Lang’ata almaarufu Jalang’o, John Kiarie wa Dagoretti Kusini, Beatrice Elachi wa Dagoretti Kaskazini, na Ronald Karauri wa Kasarani miongoni mwa wengine.
Karauri alihamia UDA siku chache zilizopita na anawinda kiti cha Ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu ujao.

Mkutano huo ulilenga kupanga mikakati ya namna ya kukabiliana na uchaguzi mkuu wa mwaka ujao wakati wapinzani wakiimarisha jitihada za kuibandua serikali ya Kenya Kwanza madarakani.
Nao umekuja wakati ambapo kura ya hivi punde ya maoni inaonyesha kinara wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna huenda akatoa ushindani mkali kwenye uchaguzi huo.
Rais Ruto amesema haijalishi ni nani atakuwa mpinzani wake, ataibuka mshindi katika uchaguzi huo asubuhi na mapema.