Viongozi wa makanisa ya Kipentekote wataka haki kwa Ojwang’

Aidha viongozi hao wa kidini wamemtaka Rais William Ruto, kuhakikisha kukomeshwa kwa mauaji ya kiholela nchini na polisi ,uovu ambao umekuwa ukitekelezwa na maafisa wa polisi kwa muda mrefu.

Dismas Otuke
1 Min Read

Chama cha makanisa ya Kipentekote (PVK),nchini kimetaka kusitishwa kwa muaji ya kiholela nchini yanayotekelezwa na polisi na kutendewa kwa haki kwa Mwanablogu Albert Ojwang’, aliyeuawa na polisi akiwa korokoroni .

Wakizungumza na Wanahabari Jumamosi,mwenyekiti wa chama hicho cha PVK ,Kasisi Peter Manyuru, ametaka uchunguzi wa haraka na tume huru ya kutathimini utendakazi wa maafisa wa polisi  (IPOA),  kuhusu mauaji ya kinyama ya Ojwang’ na waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Tunataka IPOA ifanye uchunguzi wa haraka na wa kina na kuwachukulia hatua wote waliohusika kwa mauaji hayo,”akasema Askofu Manyuru

Aidha viongozi hao wa kidini wamemtaka Rais William Ruto, kuhakikisha kukomeshwa kwa mauaji ya kiholela nchini na polisi ,uovu ambao umekuwa ukitekelezwa na maafisa wa polisi kwa muda mrefu.

Kasisi Manyuru pia amewataka vijana wanaofanya maandamano kupinga mauaji hayo ya Ojwang’, kujiepusha na vurumai na uharibifu wa mali.

“Maandamano ni haki iliyo kwenye katiba kwa kila Mkenya,ila tunaona wahuni wameingilia maandamano hayo ya vijana yenye nia nzuri,tunawaomba vijana wa Gen Z, wadumishe amani na kujiepusha na uharibifu wa mali.”akasema Akosfu Manyuru.

Haya yanajiri huku afisa mkuu wa kituo cha Polisi cha Central na Samson Talaam, na Polisi aliyeripotiwa kuwa kwa zamu kukamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Website |  + posts
Share This Article