Viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza katika kaunti ya Kwale wakiongozwa na Gavana Fatuma Achani wamedai kwamba maandamano yaliyoshuhudiwa hivi maajuzi katika eneo la Diani na mengine yalidhaminiwa na walioshindwa kwenye uchaguzi mwaka 2022 na wanaharakati.
Inadaiwa kwamba watu wenye ushawishi mkubwa na walio na mvuto wa kisiasa kutoka kaunti jirani ya Mombasa wanahusika kwenye ufadhili huo.
Huku akilaani maandamano hayo ambayo anasema yalisababisha uharibifu mkubwa Gavana Achani aliyezungumza wakati wa kugawa hundi za ufadhili wa masomo kutoka kwa hazina ya maendeleo ya eneo bunge la Msambweni alisema maandamano yaliwapa fursa wahuni kuvamia wakazi na watalii huko Diani.
Achani alisisitiza kwamba kaunti ya Kwale sio kaunti ndogo ya Mombasa na hivyo watu wa nje hawaruhusiwi kuingilia masuala ya kaunti hiyo chini ya uongozi wake.
Mashirika ya uanaharakati yanayotekeleza shughuli katika kaunti ya Kwale yalionywa vikali na gavana huyo akisema mengi yalitumiwa kudhamini maandamano ambayo yalisababisha uharibifu mkubwa katika eneo la kiuchumi la kaunti ya Kwale.
Achani alifichua kwamba alikuwa amehimiza wabunge wa kaunti hiyo kuunga mkono mswada wa fedha wa mwaka 2024 bungeni ikitizamiwa changamoto zinazokumba kaunti ya Kwale ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.
Mbunge wa Msambweni Feisal Badar kwa upande wake alisema hajutii kuunga mkono mswada huo, kwani alifanya hivyo kwa sababu ya maslahi ya kaunti ya nzima ya kwale.