Viongozi wa Kaskazini Mashariki wapongeza hatua ya kuondolewa kwa hitaji la ukaguzi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa mazingira Aden Duale.

Viongozi kutoka Kaskazini Mashariki mwa nchi, wamepongeza hatua ya Rais William Ruto, ya kuondoa hitaji la kufanyiwa ukaguzi kabla ya kupewa kitambulisho cha taifa kwa wakazi wa eneo hilo.

Wakiongozwa na waziri wa mazingira Aden Duale, viongozi hao walidokeza kuwa hatua hiyo itachangia pakubwa katika kushughulikia madhila ya kihistoria yaliyowakumba wakazi hao.

Kulingana na Duale, kwa muda wa miaka mingi, jamii zinazoishi mpakani hususan katika kaunti zilizo Kaskazini Mashariki mwa nchi, zimekumbwa na changamoto kupata kitambulisho cha taifa.

“Mchakato wa ukaguzi na hitaji la kuwa na stakabadhi zaidi, zilichelewesha upatikanaji wa kitambulisho cha taifa na kuzidisha ubaguzi na hivyo kuhujumu haki za wakenya hao,” alisema Duale.

“Mageuzi haya ambayo yamesubiriwa kwa muda mrefu, ni ushindi mkubwa kwa ujumuishaji, kuhakikisha kila mkenya bila kujali sehemu alikozaliwa, anapata haki sawa bila vizuizi,” aliongeza waziri huyo.

Alisema hatua hiyo ya Jumatano inasherehekewa na wakazi hasa walee wanaoishi mipakani ambao wamekumbwa na changamoto kubwa kupata stakabadhi hiyo muhimu.

Huku akitoa agizo hilo, Rais William Ruto alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa utawala wake kutekeleza umoja wa kitaifa na maendeleo katika maeneo yaliyotengwa.

TAGGED:
Share This Article