Makumi ya viongozi kutoka kote duniani wanakutana nchini Azerbaijan leo Jumanne kwa mkutano wa tabia nchi wa COP29. Lakini viongozi mashuhuri wanakosa kuhudhuria mkutano huo ambako athari ya ushindi wa Donald Trump kama Rais wa Marekani inadhihirika.
Viongozi zaidi ya 75 wanatarajiwa katika mji mkuu wa Baku katika kipindi cha siku mbili zijazo, lakini wakuu wa baadhi ya nchi mashuhuri zaidi zinazochangia uchafuzi wa hewa hawatahudhuria mkutano wa mwaka huu.
Ni viongozi wachache tu wa Kundi la Nchi zilizostawi zaidi kiuchumi duniani G20 — ambazo zinachangia karibu asilimia 80 ya gesi chafuzi kwa mazingira duniani — wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. Miongoni mwao ni Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Joe Biden, Xi Jinping, Narendra Modi na Emmanuel Macron ni miongoni mwa viongozi watakaokosa kuhudhuria mkutano huo, ambako wasiwasi juu ya ushirikiano wa Marekani katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi umetanda siku ya kwanza ya ufunguzi wa mkutano huo.
“Siyo hali inayostahiki,” alikiri Steven Guilbeault, Waziri wa Mazingira wa Canada.
“Lakini katika kipindi cha miaka 30 ya mkutano huu wa tabia nchi, si mara ya kwanza tumekumbana na vizuizi,” aliiambia AFP.
“Bila shaka, kila kitu bado kinawezekana.”