Viongozi Mandera wakana madai ya wenyeji kufurusha walimu

Marion Bosire
1 Min Read

Viongozi wa kaunti ya Mandera wamekanusha madai kwamba wenyeji hushirikiana katika kufurusha walimu wasio wenyeji wa kaunti hiyo.

Walisema kundi la kigaidi la Al-Shabaab ambalo husababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo ni tishio hata kwa wenyeji na kwamba wazaliwa wa eneo hilo wamepoteza maisha mikononi mwa magaidi wakitetea walimu ambao sio wenyeji.

Gavana wa Mandera Mohamed Khalif, wakati akiwahutubia wenyeji kwenye hafla ya kuzindua utoaji wa chanjo ya kipindupindu, alionyesha kutoridhika na madai ya viongozi fulani kwamba wenyeji wanashirikiana na kundi la Al-Shabaab.

Kulingana naye, kundi hilo ni tishio kwa ulimwengu wote na ni muhimu kuungana katika juhudi za kulikabili.

Gavana Khalif alisisitiza umuhimu wa kujitolea wakati wa kutuma maombi ya kazi hasa za ualimu katika eneo hilo. Alikosoa walimu ambao hutuma maombi ya kazi katika eneo la kaskazini mashariki na baada ya siku chache wanaomba uhamisho kutokana na ukosefu wa usalama.

Mwakilishi wa kaunti ya Mandera bungeni Ummulkheir Kassim, alitumia fursa hiyo kuhimiza wenyeji kusomea kozi za ualimu akisema wakati umewadia wa watoto wa eneo hilo kufunzwa na walimu wenyeji.

Anaonelea kwamba hatua hiyo ndiyo suluhisho kwa madai ya wenyeji kudhuru walimu wasio wenyeji na kudhihirisha kujitolea kwao katika kuendeleza elimu na maendeleo ya jamii.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *