Wanasiasa watano wanahojiwa kuhusiana na ghasia zilizoshuhudiwa kaunti ya Tana River, ambazo hadi sasa zimesababisha vifo vya watu 19.
Viongozi hao kwa sasa wako katika afisi za tume ya kitaifa ya mshikamano na maridhiano NCIC.
Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia alipokuwa akizungumza katika mkutano na chama cha wahariri leo Jumatatu, alithibitisha kuwa watano hao ni pamoja na mwakilishi wanawake wa kaunti hiyo Amina Dika Abdullahi, aliyekuwa mwakilishi wanawake wa kaunti hiyo Rehema Hassan, mbunge wa Bura Yakub Adow Kuno, mbunge wa Galole Hiribae Said Buya, na mwakilishi wadi ya Bangale Jibril Mahamud Farah.
Kobia alidokeza kuwa yeye pamoja na makamishna wengine wawili wa tume hiyo, walizuru kaunti ya Tana River kukadiria hali ilivyo.
Kulingana na mwenyekiti huyo, tume ya NCIC kwa ushirikiano na asasi zingine za serikali, zimeanzisha uchunguzi kuhusu ghasia hizo za kijamii, ambazo pia zimesababisha baadhi ya wakazi kutoroka makwao.
Nyumba kadhaa zimeteketezwa katika mashambulizi hayo kati ya jamii hasimu.