Shirikisho la mchezo wa Karate nchini limerai serikali kujumuisha mchezo wa Karate katika mtaala wa elimu – CBC kwa faida ya ujuzi wa kujilinda.
kwa mijibu wa rais wa shirikisho hilo mhandisi Richard Minga, ujuzi huo utawafaidi wanafunzi hao katika utimamu wa kimwili, nidhamu na kuzuia magonjwa kama vile fetma.
Akizungumza mjini thika katika mkutano wa maandalizi ya kidumbwedumbwe cha Jumuiya ya madola cha mchezo huo nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 28/11 – 1/12/2024, Minga aliongeza kuwa, baadhi ya shule hucheza mchezo huo kama shughuli za ziada za mtaala wa elimu kama ilivyo mchezo wa kuigiza na skauti.
Pia alisema kuwa ujuzi huo wastahili kuwa wa lazima kwa vikosi vya usalama nchini kama vile polisi kwa sababu askari aliye na ujuzi huo ana uwezo wa kukabili waandamanaji na makundi ya watu wenye ghadhabu.
Naye mmoja wa wachezaji wa mchezo huo Joyce Juma, alisema kuwa ana imani timu ya taifa itashinda medali lukuki katika mashindano hayo ila akataja fedha na vifaa vya mazoezi kama changamoto kuu na ambayo imelemaza mchezo huo nchini. ” Tunahitaji fursa nyingi za kufanya mazoezi pamoja, na muhimu zaidi ufadhili ili kukuza ujuzi wetu”, Alisema Joyce.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mweka hazina wa kitaifa wa mchezo huo nchini Muthanga Ndegwa aliye iomba serikali na wafadhili wengine kufadhili timu ya taifa.
kwa upande wake, mkufunzi Gladys Ndinda, alionyesha furaha yake kwa ongezeko la akina dada wanaoshiriki Karate.
” Wanawake wengi wanakumbatia na kufanikiwa katika Karate kama wanaume”, Alifichua Ndinda.