Vijana katika kaunti ya Kajiado wametakiwa kukumbatia kilimo biashara ili kukabiliana na ukosefu wa ajira na kuimarisha usalama wa chakula.
Kulingana na Paul Mbugua ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi ya Kilimo Biashara ya Latia, sekta ya kilimo ina fursa kubwa ya kubuni nafasi za ajira kwa mamia ya vijana wasiokuwa na ajira na kuboresha hali yao ya maisha.
Mbugua ametoa changamoto kwao kubadili dira na kusomea kozi zinazohusiana na kilimo na uzalishaji wa chakula ili kupata ujuzi utakaowawezesha kuanzisha miradi yao ya kilimo na hivyo kujiajiri.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa mkakati wa taasisi hiyo uliofanyika katika kaunti ya Kajiado.
“Kuna fursa nyingi katika sekta ya kilimo. Hapa Latia, tunatilia mkazo uhamasishaji wa vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kubuni nafasi za ajira na kuimarisha usalama wa chakula,” aliongeza Mbugua.