Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Veronica Mueni Nduva, aliapishwa kuchukua wadhifa huo Ijumaa jioni katika Ikulu ya Rais Jijini Juba, Sudan Kusini.
Nduva aliapishwa wakati wa mkutano wa 23 wa viongozi wa serikali ulioandaliwa kwa njia ya mtandaoni na ambao uliongozwa na Rais Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit, aliye mwenyekiti wa mkutano huo.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Nduva alisema atatumia muhula wake kuimarisha zaidi utangamano na maendeleo ya raia wa Afrika Mashariki.
Nduva alisema atapatia umuhimu kuboresha utangamano wa kiuchumi unaochochea ubunifu, ujasiriamali na kubununi nafasi za ajira, usalama na udumishaji amani.
“Kwa kuhakikisha amani na usalama, Afrika Mashariki ni msingi wa kujenga ustawi wa kudumu,” alisema Nduwa.
Nduva, ambaye ni katibu mkuu wa kwanza mwanamke wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alidokeza kuwa ustawi wa kijamii ni muhimu akisema atashinikiza kuwezeshwa kwa wanawake na vijana ambao aliwataja ndio uti wa mgongo wa jamii ya eneo hilo.
Aidha alisema ataendelea na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi katika kanda hii, ikiwa ni pamoja na kupigia debe utumizi wa kawi safi, uhifadhi wa mazingira na kilimo endelevu.