Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani aliongoza hafla ya kuzindua mradi wa kuweka taa za barabarani zinazotumia miale ya jua katika maeneo ya Ukunda na Bongwe/Gombato.
Taa hizo zitawekwa kwenye barabara kati ya Tandoori na hoteli ya Baobab beach katika wadi ya Ukunda na barabara kati ya benki ya ABSA na hoteli ya Jacaranda.
Mradi huo unalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa umma katika maeneo yaliyo karibu na ufuo wa bahari ambao ni kitega uchumi kwa wakazi wengi wa kaunti ya Kwale.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Gavana Achani alisisitiza umuhimu wa kuimarisha riziki kwa kuimarisha mazingira ya kazi, akigusia jinsi mradi huo utatatua wasiwasi wa muda mrefu wa usalama wa watalii, watumizi wa fuo na wakazi.
Taa hizo zitaimarisha sio tu usalama bali pia zitachangia ukuaji wa biashara, utunzaji wa mazingira na ufanisi wa nishati.
Wakazi wamekuwa wakiibua wasiwasi kuhusu ukosefu wa usalama katika eneo hilo huku ripoti za wizi na visa vingine vya uhalifu zikitolewa hasa katika maeneo ambayo hayana mwangaza.
Gavana huyo alihakikishia wakazi kuhusu kujitolea kwa serikali yake kwa utoaji huduma akisema hawatoi ahadi tu bali pia wanachukua hatua.
“Huu ndio mwanzo tu wa miradi mingi inayolenga kuboresha maisha ya watu wetu.” aliongeza kusema Gavana Achani.
Viongozi wengine waliokuwepo waliwataka wakazi kuwa macho na kulinda miundombinu hiyo mipya dhidi ya kuharibiwa.
Mwakilishi wa wadi ya Bongwe/ Gombato Tumaini Mwachaunga, aligusia visa vya mali ya umma kuharibiwa kama vile taa za barabarani.
“Tushirikiane kulinda uwekezaji huu kwa manufaa ya kila mmoja wetu.” alisema Mwachaunga.
Wakazi walishukuru serikali ya kaunti kwa kusikia kilio chao na kuchukua hatua. Mwakilishi wa wakazi wa eneo hilo kwa jina Mokaya alisema wamekuwa wakiogopa kupita sehemu fulani usiku lakini sasa serikali ya kaunti imeweka taa.
Mradi huo wa taa za barabarani zinazotumia miale ya jua ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kuimarisha usalama, miundombinu, nishati ya kijani na ubora wa maisha ya wakazi wa Kwale.