Maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Rais Donald Trump walielezea mipango ya kina ya mashambulizi ya kijeshi nchini Yemen kwa kikundi kimoja cha mawasiliano ambacho kwa bahati mbaya kinamjumuisha mhariri mkuu wa jarida la Atlantic la Marekani.
Mhariri Mkuu wa jarida hilo Jeffrey Goldberg anasema alipokea ombi la kujiunga kwenye huduma ya kutumiana ujumbe ya Signal tarehe 11 mwezi huu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama Mshauri wa Usalama wa Taifa Mike Waltz.
Goldberg anasema baadaye aliongezwa kwenye kikundi cha mawasiliano ambacho kilijumuisha maafisa wakuu wa usalama wa taifa wa utawala wa Rais Trump.
Kulingana na mhariri huyo, mtu aliyemdhania kuwa ni Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth alituma taarifa za operesheni ya mashambulizi yaliyotarajiwa kutekelezwa dhidi ya vikosi vya Houthi nchini Yemen.
Ripoti zinaashiria kuwa hii ilijumuisha taarifa juu ya maeneo lengwa na silaha za kutumiwa katika mashambuliizi hayo.
Goldberg anaongeza kuwa mashambulizi ya Machi 15 yalifanyika yamkini saa mbili baada ya yeye kupokea ujumbe kuhusu mipango hiyo.
Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya Marekani limesema kwenye taarifa kuwa mazungumzo ya kikundi hicho “yanaonekana kuwa ya kweli.”
Hata hivyo, kuvuja kwa taarifa hizo kumeibua mashaka juu ya namna utawala wa Rais Trump unavyoshughulikia taarifa za siri.