Ureno yafuzu kwa awamu ya pili ya Euro

Marion Bosire
2 Min Read

Timu ya Ureno imetinga raundi ya 16 ya mashindano ya mataifa bingwa barani Ulaya kwa kuizaba Uturuki magoli matatu kwa nunge ugani Signal Iduna Park.

Mabao hayo yalipachikwa wavuni na Bernardo Silva wa klabu ya Manchester City, Samet Akaydin ( aliyejifunga) na Bruno Fernandes wa klabu ya Manchester United namo dakika ya 21, 28 na 55 mtawalia.

Vile vile kwenye kundi hilo la F, Georgia na Czechia walitoshana nguvu ya goli moja kwa moja uwanjani Volkspark. Georges Mikautadze na Patrik Schick walifungia Georgia na Czechia dakika ya 45+4 na 59 mtawalia.

Kwenye jedwali, Ureno imo kileleni kwa alama sita wakifuatwa na Uturuki, Czechia na Georgia kwa alama tatu, moja na moja mtawalia.

Kwenye kundi E, Ubeligiji kupitia Youri Tielemans wa klabu ya Aston Villa na nahodha Kevin De Bruyne wa klabu ya Manchester City, waliilaza Romania mabao mawili kwa nunge ugani SRheinEnergie. Mawili hayo yalitiwa kimyani dakika ya 2 na 59.

Leo jumapili kutachezwa mechi mbili za mwisho za kundi A saa nne usiku. Ujerumani watakabana koo na Uswizi ugani Deutsche Bank Park wakati Scotland wakizichapa na Hungary uwanjani MHP.

Katika kundi hilo Ujerumani wanaongoza kwa alama sita. wanafuatwa na Uswizi, Scotland na Hungary kwa alama nne, moja na sufuri mtawalia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *