Matumaini ya klabu ya Simba kuwaandaa RS Berkane ya Morocco ,katika uwanja wa Benjamin Mkapa, marudio ya fainali ya Kombe la Shirikisho yameyeyuka baada ya CAF ,kuthibitisha kuwa mkwangurano huo utakasatwa katika uchanjaa wa Amaan kisiwani Zanzibar.
Kwenye waraka wa CAF kwa shirikisho la kandanda nchini Tanzania TFF, muda mfupi wa kukagua na kuidhinisha uwanja wa Mkapa ndicho chanzo cha kukosa kutoa idhini matumizi ya uga huo wa Dar.
CAF imeongeza kuwa inaendelea na ukaguzi wa uwanja wa Mkapa pamoja na vile vya Kenya na Uganda kuhakikisha viko tayari kwa michuano ya CHAN.
Simba waliocharazwa mabao 2-0 katika duru ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na Berkane Jumamosi iliyopita, walitarajia wangesaidiwa na mashabiki wa nyumbani kwa Mkapa kupindua meza.
Simba inashiriki fainali ya kombe hilo kwa mara ya kwanza, na ni miaka miwili tu tangu watani wao Yanga kupigwa fainalini na USM Alger ya Algeria.
Mshindi wa Kombe hilo atatuzwa dola milioni 2 huku mshindi akiondoka na dola milioni 1.