Timu za Ureno na Uturuki zilihitimisha awamu ya kwanza ya mechi za makundi ya kipute cha bara Uropa kinachoendelea nchini Ujerumani kwa ushindi dhidi ya Czechia na Georgia mtawalia.
Kwenye mtanange wa jana Jumanne saa nne usiku ugani Red Bull Leipzig, nahodha Christiano Ronaldo aliwaongoza nyota wenzake kama vile Bruno Fernandes (Manchester United) na Bernado Silva (Manchester City) miongoni mwa wengine kuipa Ureno ushindi wa magoli mawili kwa moja.
Mchuano huo ulikuwa wa kasi huku kila timu ikibisha. Ni kupitia hodihodi hizo ambapo Lukáš Provod aliiweka Czechia uongozini dakika ya 62. Baada ya dakika saba, Ureno ilinoa makali yaliyomsababisha beki Robin Hranáč kujifunga.
Timu zote ziliendelea kufanya mashambulizi ila Ureno wakabahatika kupata ushindi kupitia bao la Francisco Conceição mnamo dakika ya 90+3.
Kwenye mechi ya awali uwanjani Signal Iduna Park, Uturuki iliipepeta Georgia magoli matatu kwa moja, matatu hayo yalitiwa wavuni na Mert Müldür, Arda Güler na Muhammed Kerem Aktürkoğlu dakika ya 25, 65 na 90+7. Nalo bao la pekee la Georgia lilitingwa kimiani na winga Georges Mikautadze dakika ya 32.
Kufuatia matokeo hayo ya kundi F, jedwali linaongozwa na Uturuki kwa alama tatu sawia na Ureno walio na uchache wa mabao.
Czechia na Georgia wamo nafasi ya tatu na nne mtawalia. Kipute hicho kitaingia awamu ya pili hii leo Jumatano pale Luka Modric atakapoiongoza Croatia kuikabili Albania saa kumi jioni.
Wenyeji Ujerumani watacheza na Hungary saa moja usiku kisha Scotland wakabane koo na Uswizi saa nne usiku.