Hospitali ya kitaifa ya Muhimbili nchini Tanzania imeandikisha historia ya kuwa hospitali ya kwanza ya umma kutekeleza upasuaji wa kupunguza uzani wa mwili kwa watu wanne.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo ya Muhimbili Profesa Mohamed Janabi amesema upasuaji huo ulitekelezwa kwa utaalamu wa hali ya juu ambapo wote waliofanyiwa hawakupasuliwa bali walitumia endoskopia kuingia katika tumbo na kupunguza sehemu ya tumbo la chini na pia kutumia matundu madogo.
Prof. Janabi amesema huduma hii imehusisha Wataalamu wa Hospitali ya Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka nchini India, Dkt. Mohit Bhandar pamoja na Taasisi ya MedINCREDI.
Katika muda wa mwaka mmoja, mtu aliyefanyiwa upasuaji huo anaweza kupunguza uzani kwa kilo 20 hadi 30.
“Tuliowafanyia huduma hii wana umri wa kati ya miaka 36-40, ambao uzito wao ni kati ya kilo 107 hadi 142, mmoja aliruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya masaa manane na wengine watatu wakaruhusiwa siku iliyofuata hivyo ukifanyiwa huduma hii haikuzuii kurudi katika majukumu yako kwa wakati.” alielezea Janabi.
Profesa Janabi ameshauri Jamii kujikinga kupata uzito uliopitiliza kwa kuepuka kula mara kwa mara kwa kuwa uzito unaweza kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ambayo gharama ya matibabu ni ghali.