Baraza la Magavana (CoG) limetishia kusitisha utoaji huduma kwenye kaunti katika kipindi cha siku 30 zijazo ikiwa serikali kuu haitatoa mgao wa fedha zinazodai kaunti hizo ili kuhakikisha utendaji kazi wake.
Baraza hilo limetoa tishio hilo leo Jumatatu wakati wa mkutano usiokuwa wa kawaida ulioitishwa kuangazia masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na Mswada wa (Marekebisho) wa Ugavi wa Mapato 2024 na ukawiaji katika kutoa fedha kwa kaunti.
Mkutano huo uliongozwa na mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi.
Magavana wamekuwa wakiinyoshea serikali kuu kidole cha lawama kwa kukawia kutoa kwa kaunti mgao wa fedha katika hatua ambayo imeathiri utoaji huduma kwa raia kwa kiwango kikubwa.
Tishio lao linakuja wakati Bunge la Taifa na lile la Seneti yametofautiana kuhusiana na kiasi cha fedha zinazopaswa kutolewa kwa kaunti.
Huku Seneti ikitaka kaunti kupewa mgao wa takriban shilingi bilioni 400, Bunge la Taifa linashikilia kuwa ni shilingi bilioni 380 zinazoweza kutolewa kwa kaunti.
Hali hiyo imemfanya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kutoa wito kwa mabunge hayo mawili kusuluhisha tofauti zao na fedha kutolewa haraka iwezekanavyo kwa kaunti ili kutolemaza utoaji huduma kwa raia.