Uingereza na Uholanzi watamba

Marion Bosire
2 Min Read

Timu ya Uingereza na Uholanzi walianza vyema kampeni ya kusaka taji la Uropa katika kinyanganyiro kinachoendelea nchini Ujerumani kwa kulaza Serbia na Poland mtawalia.

Kwenye mchuano wa kundi chaa (C) uliosakatwa saa nne usiku ugani Veltins, Uingereza walimakinika na kupata bao la pekee la mchuano huo katika dakika ya 13 kupitia Jude Bellingham wa klabu ya Real Madrid. Licha ya kujisatiti kwa makombora, Serbia walikosa bahati hivyo kupelekea mchuano huo kuisha kwa bao moja.

Mechi nyingine ya kundi hilo baina ya Denmark na Slovenia pale uwanjani MHP, iliishia sare ya bao moja kwa moja.Denmark walipata bao kupitia Christian Eriksen wa klabu ya Manchester United namo dakika ya 13 huku Erik Janža akiisawazishia Slovenia dakika ya 77.

Kundi hilo linaongozwa na Uingereza kwa alama tatu huku Denmark, Slovenia na Serbia wakifuata kwa alama moja, moja na sufuri mtawalia.

Hapo awali kwenye kundi daa (D), Uholanzi waliipiku Poland kwa mabao mawili kwa moja ugani Volkspark. Poland walitangulia kutikisa wavu kupitia Adam Buksa katika dakika ya 16. Dakika ya 29, Cody Gakpo wa klabu ya Liverpool alisawazisha kisha Wout Weghorst akaipa Uholanzi la pili kwenye dakika ya 83.

Jedwali kamili la kundi hilo litajiri hii leo pale Ufaranza watakapomenyana na Austria saa nne usiku.

Ngarambe zingine zitakazo pepetwa hii leo ni zile za kundi E kati ya Romania na Ukraine saa kumi jioni na Ubeligiji dhidi ya Slovakia saa moja usiku.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *