Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali wale wanaomkosoa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kutangaza kufutilia mbali ufadhili wa mipango ya afya katika nchi mbalimbali duniani.
Uhuru badala yake amesema hatua ya Trump inapaswa kuwazindua viongozi wa mataifa husika kuwa wanapaswa kutafuta njia bora za kufadhili mipango yao ya afya badala ya kutegemea ufadhili.
“Niliona watu wengine siku iliyopita wakilia kwamba Trump ameondoa pesa, amesema hatupi fedha zaidi. Watu wanalia, mbona mnalia? Hiyo siyo serikali yako, siyo nchi yako, hana sababu ya kukupa chochote! Haulipi ushuru Marekani, anafurahisha watu wake, shauri yenu Bwana,” alisema Uhuru.
“Hii inapaswa kuwazindua ili mseme ni nini tutakachokifanya ili kujisaidia? Badala ya kulia, tujiulize tunaenda kufanya nini? Ameondoa hiyo pesa, sasa tutafanya namna gani jamani? Wakati umewadia wa sisi kutumia rasilimali zetu kwa vitu vinavyostahiki.”
Uhuru alikuwa akizungumza wakati akihutubia Mkutano wa Usalama wa Afya Duniani wa Kanda ya Afrika Mashariki jijini Mombasa leo Jumatano.
Mkutano huo unawaleta pamoja viongozi na wataalam wa afya kuangazia namna ya kukabiliana na changamoto za usalama wa afya katika kanda hiyo.
Maoni yake yanakuja wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuiondoa nchi hiyo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) katika hatua ambayo wengi wanahofia itaathiri usimamizi wa masuaa ya afya kote duniani.
Aidha, Trump ametangaza kusitishwa kwa ufadhili wa mipango ya kukabiliana na maradhi kama vile Ukimwi na kifua kikuu katika hatua ambayo hasa itaathiri mataifa mengi yanayoendelea ikiwemo Kenya.