Uganda kuandaa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili mwaka 2025

Dismas Otuke
2 Min Read

Uganda imeteuliwa kuwa mwandalizi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili mwaka ujao.

Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afrika Mashariki Fest Dkt. Kisembo Ronex Tendo.

Amezungumza hayi akiwa jijini Havana nchini Cuba kwenye Kongamano la Kimataifa la Kiswahili, lililoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya usimamizi wa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole.

Dkt. Tendo alisema kuwa tarehe rasmi za kongamano hilo mwakani zitatangazwa hivi karibuni kwenye kikao cha waandishi wa habari jijini Kampala.

“Kiswahili ni fahari yetu, tunapaswa kujivunia kukiendeleza na kukieneza maana ni lugha unganishi, isiyobagua na ni lugha wezeshi kibiashara,” alisema Dkt. Tendo

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amefurahikia tangazo hilo akisema kuwa ni jambo la kujivunia.

Kulingana na Dkt. Tendo, lengo kuu la kongamano hilo la mwaka ujao, ni kubadili fikra ya chuki na kutojali miongoni mwa Waganda kuhusu kupokea na kutumia lugha ya Kiswahili kwenye maisha yao ya kawaida ikiwemo mazungumzo na kufanya biashara.

“Kiswahili kinajikita kwenye nguzo moja wapo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni kuwepo kwa Soko huria na la wazi kwa Wanajumuiya ya Afrika Mashariki.”

Ameongeza kuwa kwa vile Kiswahili ndio lugha rasmi inyotumika na wafanyabiashara, Waganda hawana budi kubadili mtazamo na fikra na kukikumbatia Kiswahili katika shughuli zao za kila siku.

“Hatuwezi kuendelea kushikilia chuki zilizosababishwa na vita vya Kagera mwaka 1979. Kwa hivyo kama Waganda tusipojipanga, tutabaki nyuma kwa mshangao. Kiswahili sio lugha ya wezi, wanyanyasaji, wahuni wala wabakaji, bali ni farari yetu ambayo tunapaswa kujivunia,” alisema Dkt Tendo.

Kongamano la Kimataifa la Kiswahili liliandaliwa kati ya tarehe 7 na 10 mwezi huu mjini Havana, Cuba na kuwaleta pamoja wajumbe wa mataifa yanayozungumza Kiswahili ikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania na kisiwa cha Unguja.

Kongamano la Kimataifa la Kiswahili la mwaka huu ni tukio lenye hadhi ya kidunia, linaloandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Cuba na Wadau wa Kiswahili Duniani kwa lengo la kukuza, kuenzi na kueneza lugha ya Kiswahili.

Share This Article