Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema juhudi za kimataifa za kujaribu kuishawishi nchi yake, hazitafaulu.
Kauli za Rais Museveni zinajiri yapata zaidi ya juma moja baada nchi yake kuondolewa kwenye mpango maalum wa biashara baina ya Marekani na bara Afrika.
Awali Marekani ilitishia kuiwekea Uganda vikwazo na kuiondoa kutoka mkataba wa ukuzaji bara Afrika-Agoa mnamo mwezi Mei baada ya Uganda kupitisha sheria tata inayopinga ushoga.
Sheria hiyo inapendekeza hukumu ya kifo kwa vitendo vya ushoga.
Rais Museveni akiongea kwa mara ya kwanza tangu kuondolewa kwa nchi yake, alisema Uganda sasa inaangazia kukabiliana na ufisadi ambao ndilo tatizo kubwa linalokabili nchi hiyo.
Museveni alisema kwamba Uganda itashirikiana kibiashara na wadau wa kimataifa wanaoiheshimu.
Uganda pia ilikaza kamba sheria yake ya kupinga ushoga mwezi Agosti, wakati benki ya dunia ilisimamisha ufadhili wake kwa nchi hiyo, ikidai sheria hiyo ni kinyume cha kanuni zake.