Uenyekiti wa AUC: Raila ageukia maombi kabla ya uchaguzi

Martin Mwanje
1 Min Read
Raila Odinga - Mgombea wa uenyekiti wa AUC

Ikiwa imesalia chini ya wiki moja kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amegeukia maombi. 

Wakuu wa Nchi wa bara la Afrika wanatarajiwa kukongamana jijini Addis Ababa nchini Ethiopia mwishoni mwa wiki hii kumchagua mwenyekiti mpya wa AUC atakayemrithi  Moussa Faki Mahamat ambaye muhula wake wa kuhudumu unamalizika.

Maombi ya kumtakia kila la heri Raila yamefanyika leo Jumatatu katika ukumbi wa Bomas katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Maombi hayo yanakuja saa chache baada ya maombi sawia kuandaliwa na wafuasi wa chama cha ODM mjini Kakamega.

Katika azma yake ya kuwania uenyekiti wa AUC, Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Madagascar Richard Randriamandrato.

Mwanawe Rais wa zamani wa Tanzania, Jospeh Magufuli, Jessica Magufuli alitua jijini Nairobi kumtakia Raila kila la heri katika safari yake ya kuwinda uenyekiti wa AUC.

 

Website |  + posts
Share This Article