Taasisi ya Wahandisi nchini – IEK, imeitaka serikali kujali maslahi ya wahandisi wa mashirika ya serikali yatakayofungwa au kujumuishwa.
Hii inafutaia tangazo la serikali baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri katika kaunti ya Kakamega tarehe 21 mwezi jana, kuhusu mashirika yatakayofungwa au kujumuishwa ili kuboresha utoaji huduma na kuimarisha utendakazi.
Rais wa IEK Mhandisi Shammah Kiteme, amesema ipo haja kwa serikali kuzingatia usawa wakati wa kuwahamisha wanachama wake walioathiriwa na agizo hilo.
Kiteme amesema wahandisi watakaohamishwa au kupewa majukumu mapya wanapaswa kupewa majukumu sawia na waliyokuwa nayo awali na pia marupurupu na mishahara inapaswa kudumishwa au kusawazishwa na ile ya wahandisi wengine katika afisi mpya watakazohamia.
Rais huyo ametaka kutokuwa na ubaguzi wala ufisadi katika mchakato wa kuwapa wanachama wake majukumu mapya na kuyapa kipaumbele maslahi yao.
Kadhalika ametaka mchakato wa kutathmini wahandisi na kuwahamishia afisi mpya kuongozwa na jopo au mashirika huru.
Kulingana na agizo la serikali, mashirika 40 yatapunguzwa hadi 20, tisa yakifungwa na majukumu yake kuhamishiwa kwa wizara huku mengine 16 yakiunganishwa na mengine sita yakiratibiwa upya.