UDA ni moto wa kuotea mbali, wasema wabunge wa Mlima Kenya

Viongozi hao wanasema ushindi wa UDA kwenye uchaguzi mdogo wa Februari 26 ni ishara kwamba chama hicho ni cha kitaifa.

Martin Mwanje
1 Min Read
Viongozi wa Mlima Kenya wakiwahutubia wanahabari Februari 27

Wabunge wa Mlima Kenya wanaogemea utawala wa Kenya Kwanza wametaja uchaguzi mdogo uliofanyika jana Alhamisi kuwa ushahidi kwamba chama UDA ni cha kitaifa. 

UDA ilizoa viti vyote vinne vilivyokuwa vikishindaniwa katika eneo bunge la Isiolo Kusini na wadi za West Kabras (eneo bunge la Malava), na zile za Muminji na Evurore katika eneo bunge la Mbeere Kaskazini.

“Tunawapongeza wagombe wa UDA Tubi Mohamed Tubi, Dancun Muratia, Peter Njiru na Elphas Shalakha kwa kuibuka washindi kwenye chaguzi hizo ndogo,” walisema wabunge hao kupitia taarifa iliyosomwa na Seneta mteule Veronica Maina wakati wakiwahutubia wanahabari mapema leo Ijumaa.

“Ushindi wao ni ushahidi usioweza kupingwa wa imani ambayo Wakenya wako nayo katika uongozi wa Rais William Ruto na utawala wa Kenya Kwanza katika kuongoza taifa letu kutoka hadhi ya kiuchumi ya tatu duniani hadi hadhi ya kwanza ya kiuchumi ndani ya kizazi.”

Wabunge waliowahutubia wanahabari walikuwa wa kutoka kaunti za Kiambu, Murang’a, Meru, Embu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Tharaka Nithi, Laikipia na Nakuru.

Wameahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto licha ya madai kuwa wanakabiliwa na tishio la kufagiliwa na wimbi la chama cha DCP chake Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article