Mamlaka ya usafiri wa angani nchini KCAA imeanzisha uchunguzi kuhusu kilichosababisha ajali ya ndege huko Mosop, Nandi Hills.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wote sita waliokuwa kwenye ndege hiyo, akiwemo mbunge wa eneo la Emurua Dikirr, Johana Ng’eno.
Katika taarifa, mkurugenzi mkuu wa KCAA Emile Arao alisema kwamba wataalamu wa uchunguzi wameanzisha taratibu za kuchunguza kilichosababisha ajali hiyo.
Ndege hiyo ilianguka katika lokesheni ndogo ya Kabiyet, eneo bunge la Mosop jana saa kumi unusu jioni.
Arao anasema mamlaka ya usafiri wa angani nchini KCAA imeanzisha mipango ya kusaidia uchunguzi unaotekelezwa na kitengo cha uchunguzi wa ajali za ndege.
Ameahidi kwamba taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la jana zitatolewa kwa wakati.
Katika taarifa hiyo, Arao alithibitisha kwamba ndege hiyo ilikuwa na watu 6 wakati wa ajali na utambuzi wao na mawasiliano na familia zao ungetekelezwa na maafisa stahiki.
Mamlaka ya KCAA imetoa pole kwa familia na wapendwa wa waliohusika kwenye ajali hiyo.