Uchaguzi Mkuu: Kenya Kwanza, ODM zaunda kamati ya pamoja kuratbu manifesto

Rais William Ruto alisema kamati hiyo ambayo imejukumiwa kuratibu manifesto hiyo ya pamoja, itajumuisha wawakilishi watano kutoka kila pande.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa serikali jumuishi mjini Naivasha.

Muungano wa Kenya Kwanza na chama cha Orange Democratic Movement (ODM), vimebuni kamati ya pamoja ya kuratibu manifesto kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.

Kwenye mkutano na wanahabari baada ya mkutano wa serikali jumuishi mjini Naivasha, Rais William Ruto alisema kamati hiyo ambayo imejukumiwa kuratibu manifesto hiyo ya pamoja, itajumuisha wawakilishi watano kutoka kila pande.

Upande wa Kenya Kwanza utawakilishwa na Emmanuel Nzai, Dr Daniel Mwai, Bramwel Simiyu na Dkt. Cecilia Ng’etich, huku Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha UDA akiwa mwanachama asiye na mamlaka.

Chama cha ODM kitawakilishwa na Isaac Wanuge, Mariam Mbaruk, Leonida Kerubo na Prof. Benard Muok, huku Mkurugenzi Mtendaji wa ODM akiwa mwanachama asiye na mamlaka.

Ruto alidokeza kuwa muungano huo utakamilisha mageuzi ambayo yanaendelea kutekelezwa, huku ukibuni mpango wa pamoja kwa hatua ifuatayo ya maendeleo ya taifa.

“Kile kilichoanza kama ushirikiano serikalini, sasa utakuwa jukwaa la pamoja la kisiasa tutakalolitumia mwezi Agosti mwaka ujao,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto, manifesto itakayobuniwa itajumuisha mapendekezo yanayochipuza kutokana na mjadala wa kitaifa kuhusu ruwaza ya Kenya ya baada ya mwaka 2030, na mkataba wa kitaifa wa maendeleo.

Wakati huo huo Rais Ruto kiongozi wa ODM Oburu Oginga watabuni kamati ya pili ya wanachama watano kila kila upande, litakalojukumiwa kubuni mikakati ya makubaliano.

“Mimi na Dkt. Oburu tutawateua wanachama watano kutoka vyama vyetu vya kisiasa kubuni kamati ya pili itakayobuni miakati ya ushirikiano, itapendekeza mifumo ya uongozi itakayotoa mwongozo  wa ushirikiano wetu na kupendekeza mpangilio wa uongozi ili kupeleka mbele muugano huu,” alisema Rais Ruto.

Share This Article