Uchaguzi DRC: EAC yazuiwa kushiriki kama mwangalizi

Martin Mwanje
2 Min Read

Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC haitakuwa miongoni mwa waangalizi watakaofuatilia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC kesho Jumatano, Disemba 20,2023.

Hii ni baada ya mamlaka za nchi hiyo kukosa kuridhia ombi la EAC kushiriki uchaguzi huo kama mwangalizi.

“Hii ni kutaarifu nchi wanachama wa EAC, washiriki wa maendeleo na wadau wengine wote kwamba EAC haitakuwepo DRC kufuatilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2023 kama ilivyoelezwa katika Mkataba Ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na kama ambavyo imekuwa desturi tangu kuasisiwa kwa jumuiya hiyo,” inasema taarifa ya EAC iliyotiwa saini na Simon Peter Owaka, afisa mwandamizi wa uhusiano mwema wa umma.

“Hatua hii inatokana na ukweli kwamba ingawa EAC ilikuwa tayari, ombi la kutekeleza zoezi hilo halijakubaliwa na mamlaka husika.”

Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiongeza kuwa inaitakia serikali na watu wa DRC uchaguzi wa amani na kwamba inasalia na dhamira ya kuendelea kuzitumikia nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo.

Taarifa hiyo inakuja wakati ambapo DRC imewaita mabalozi wake nchini Kenya na Tanzania kwa “mashauriano”.

Utawala wa Felix Tshisekedi ulichukua hatua hiyo kufuatia kuzinduliwa jijini Nairobi kwa muungano ulioitwa “Congo River Alliance”.

Muungano huo uliozinduliwa Ijumaa wiki iliyopita unajumuisha wanasiasa wakuu wa DRC na wawakilishi wa makundi kadhaa likiwemo lile la waasi la M23 ambao wameteka eneo kubwa Mashariki mwa DRC.

Share This Article