Tutawasilisha mgombea mmoja dhidi ya Ruto 2027, wasema upinzani

Martin Mwanje
1 Min Read
Viongozi wa upinzani wakati wakiwahutubia wanahabari Novemba 3

Muungano wa upinzani umeahidi kuwasilisha mgombea mmoja dhidi ya Rais William Ruto wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Viongozi wa muungano huo wameelezea imani kwamba hatua hiyo itatosha kumtimua Rais Ruto madarakani.

Imekisiwa kuwa viongozi hao huenda wakashindwa kuafikiana ni nani atakayepeperusha bendera ya upinzani kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027 huku kila mmoja akimezea mate wadhifa huo.

“Ruto amesikika akijigamba kuwa ni Raila pekee ambaye angemtoa jasho 2027. Ila tunataka kumwambia kuwa upinzani hautakuwa kati yake na sisi, ila Wakenya,” alisema Naibu Rais wa zamani ambaye pia ni kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua.

“Tutazitumia chaguzi ndogo zijazo kupata mbinu ya kumtema Ruto kwenye uchaguzi wa 2027.”

Viongozi wa muungano huo wakiazimia kusimamisha mgombea mmoja mmoja katika chaguzi ndogo zijazo ikiwa ni pamoja na maeneo bunge ya Magarini, Malava na Mbeere Kaskazini ili kuhakikisha wagombea wao wanaibuka kidedea kwenye chaguzi hizo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imepanga kuandaa chaguzi ndogo katika maeneo 24 nchini Novemba 27.

Chaguzi hizo zinachukuliwa kuwa kipamajoto cha ubabe wa kisiasa kati ya serikali na upande wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Website |  + posts
Share This Article