Tume ya haki za binadamu nchini yakanusha usemi wa Rais Ruto

Marion Bosire
1 Min Read

Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu nchini, KNCHR imekanusha usemi wa Rais William Ruto kuhusu data zilizokusanywa katika eneo la Githurai, Nairobi.

Katika taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa KNCHR Roseline Odede, tume hiyo inasema imefahamishwa kuhusu usemi wa Rais Ruto wakati wa mahojiano kwamba ilitoa data gushi kuhusu mauaji ya Githurai.

Tume hiyo sasa inafafanua kwamba bado haijatoa taarifa kuhusu mauaji ya Githurai na kwamba walipotoa taarifa, walisema wazi kwamba hawakuwa na ufahamu kamili wa matukio ya maeneo ya Githurai, Rongai, Migori, Nakuru na mengine nchini.

Imeelezea pia kwamba data waliyonayo inaonyesha kwamba idadi ya vifo kutokana na maandamano ilikuwa ni 22 kufikia siku ya Jumatano walipotoa taarifa hiyo.

Kufikia jana Jumapili, tume hiyo inasema ilikuwa na ufahamu wa jumla ya vifo 24 vilivyonakiliwa tangu maandamano yalipoanza kufikia sasa.

Huku ikiahidi kuendelea kutetea haki za binadamu, KNCHR imetoa pole kwa waliofiwa na jamaa wao na kuwatakia waliopata majeraha uponyaji wa haraka.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *