Afisa Mkuu wa Polisi katika kituo cha polisi cha Rwanyambo, kaunti ya Nyandarua, amesimamishwa kazi baada ya mwanamke kujifungua akiwa kwenye korokoro za kituo hicho cha polisi.
Kupitia kwa taarifa, Huduma ya Taifa ya Polisi, ilielezea kusikitishwa na kisa hicho cha kutamausha.
“Huduma ya Taifa ya Polisi inahuzuni kubwa kufahamisha umma kuhusu kisa ambapo mwanamke alijifungua kwenye korokoro za polisi katika kituo cha polisi cha Rwanyambo, kaunti ya Nyandarua”, alisema Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga kupitia kwa taarifa.
Uchunguzi umeanzishwa na Kitencho cha Kushughulikia Maswala ya Ndani (IAU) na Halmashauri ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), kubaini chanzo cha mkasa huo.
“Ili kuhakikisha uchaguzi ulio wazi na usioegemea upande wowote, afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Rwanyambo, amesimamisshwa kazi mara moja,” alisema Msemaji huyo wa polisi.
Huduma ya Taifa ya Polisi imeelezea kujitolea kwake kuhakikisha inazingatia sheria kila wakati na kulinda haki za kibinadamu.