Trump ataka wapatanishi wa mpango wa amani Gaza waharakishe

BBC
By
BBC
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa wito kwa wanahusika wote wa juhudi za kumaliza vita vya Gaza waharakishe, wapatanishi wakitarajiwa kukutana Misri Jumatatu kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Hamas na Israel.

Mazungumzo haya yanafuatia hatua ya Hamas kukubali baadhi ya vipengele vya mpango wa amani wa Marekani wenye vipengele 20, ikiwemo kuwaachilia mateka na kukabidhi usimamizi wa Gaza kwa wataalamu wa Kipalestina.

Lakini kundi hilo hata hivyo linataka kujadili masuala mengine kwenye mpango huo.

Majibu ya kundi hilo hayakugusia madai muhimu ya kuachilia silaha na kutoshiriki tena katika uongozi wa Gaza baada ya vita.

Kupitia mitandao ya kijamii, Trump alisema kwamba mazungumzo yamekuwa ya mafanikio makubwa, akiongeza “Nimeambiwa awamu ya kwanza inapaswa kukamilika wiki hii na ninaomba kila mmoja aharakishe.”

Rais huyo wa Marekani alisema pia kwamba muda ni wa dharura, la sivyo kutakuwa na umwagaji mkubwa wa damu.

Akizungumza na waandishi wa habari awali, Trump alisema anadhani mateka wataanza kuachiwa karibuni sana.

Alipoulizwa kuhusu kubadilika kwa mpango wake wa amani, Trump alisema mabadiliko hayahitajiki kwa sababu karibu kila mtu amekubali, lakini kutakuwa na mabadiliko machache daima.

“Ni mpango mzuri kwa Israel, ni mpango mzuri kwa ulimwengu wa Kiarabu, ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima, kwa hiyo tunafurahia sana,” aliongeza.

Wakati huo huo, mashambulizi ya anga ya Israel yaliendelea Gaza, licha ya Trump kuiambia Israel kuacha mara moja mashambulizi ya mabomu siku ya Ijumaa baada ya Hamas kujibu pendekezo hilo la mpango wa amani.

Msemaji wa serikali ya Israel, Shosh Bedrosian, aliambia wanahabari Jumapili kwamba ingawa baadhi ya mashambulizi yamesimama ndani ya Ukanda wa Gaza, hakuna makubaliano ya kusitisha vita kwa sasa.

Bedrosian alisema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa amri “kujibu mashambulizi kwa madhumuni ya kujilinda ikiwa kuna tishio kwa maisha yao katika uwanja wa vita huko Gaza.”

Ripoti kutoka Gaza zinasema Israel iliendelea na mashambulizi ya anga na mizinga usiku wa kuamkia Jumapili, na kusababisha uharibifu wa majengo kadhaa ya makazi mjini Gaza.

BBC
+ posts
Share This Article