Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amemuidhinisha binti-mkwe wake kuongoza Kamati ya Kitaifa ya chama cha Republican (RNC).
Trump alionyesha uungaji mkono wake kwa Lara Trump na Michael Whatley, mwenyekiti wa chama cha Republican cha North Carolina.
Uungwaji mkono wake siku ya Jumatatu unafuatia ripoti kwamba amechukizwa na uongozi wa sasa wa RNC.
Kamati hiyo itapiga kura kwa uongozi mpya ikiwa mkuu wake wa sasa, Ronna McDaniel, atajiuzulu.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Bi. McDaniel huenda akaacha wadhifa wake baada ya uchaguzi wa mchujo wa Republican wa South Carolina, uliopangwa kufanyika tarehe 24 Februari.
RNC kama shirika inaangazia uchangishaji fedha kwa ajili ya chama na kuwaleta wafuasi wa chama cha Republican wapige kura.
Akiwa mgombeaji mkuu wa chama cha Republican katika uchaguzi wa mwaka huu, uidhinishaji wa Bw Trump huenda ukawa na ushawishi kwa wanachama wa RNC.
Katika taarifa yake ya Jumatatu jioni, Trump alisema Whatley, ambaye kwa sasa anahudumu kama mshauri mkuu wa kamati hiyo, “amefanya kazi kubwa katika jimbo lake la North Carolina” na kwamba anafaa kuwa mwenyekiti anayefuata wa RNC.