Aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump jana Alhamisi alikanusha mashtaka manne ya uhalifu dhidi yake katika mahakama ya E. Barrett Prettyman iliyoko jijini Washington DC.
Mashtaka hayo yanahusiana na kuilaghai serikali kwa kujaribu kutekeleza mpango mahsusi wa kubadili matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 kwa lengo la kusalia mamlakani.
Hii ndiyo kesi ya tatu dhidi yake tangu alipotangaza azima ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu unaopangiwa kuandaliwa Novemba 5, 2024.
Kulingana na stakabadhi za mahakama, Trump na wenzake 6, walijaribu kulazimisha watendakazi wa serikali wawasaidie kutekeleza mpango wa kusajili wapiga kura kinyume cha sheria ambao wangempigia kura Trump ili amshinde Joe Biden.
Analaumiwa pia kwa kushawishi wafuasi wake kuingia katika jengo la bunge jijini Washington D.C. Januari 6, 2021 wakati bunge lilikuwa likiidhinisha matokeo ya uchaguzi ya kiwango cha “Electoral College” na akakosa kuwaelekeza waondoke walipoingia kwa lazima kwenye afisi ya Rais.
Wakili wa Trump aitwaye John Lauro alimtetea mahakamani jana Alhamisi akisema kwamba matendo yake yote wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020 yalitokana na uhuru wa kuzungumza ambao unalindwa na sheria.
Trump alijisalimisha kwa maafisa wa polisi saa 10 kasoro robo Alhamisi jioni na kupelekwa mahakamani akiwa na mawakili wake Todd Smith na John Lauro.
Maafisa wa usalama ambao walikuwa kazini Januari 6, wakati wafuasi wa Trump waliingia kwa lazima ndani ya jengo la bunge walihudhuria kikao hicho cha mahakama.
Kabla ya hapo, Trump alikuwa amesema kwenye mitandao ya kijamii kwamba angekamatwa kwa kuzungumza dhidi ya uchaguzi uliojawa ufisadi akisema ni heshima kubwa kwake.